Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alitoa msimamo wa Tanzania
kuhusu hali ya sintofahamu inayojitokeza katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), kuwa haikusudii kujitoa wala kuwa sehemu ya lawama
iwapo jumuiya hiyo itayumba au kuvunjika.
Msimamo wa Kikwete unatokana na hali ambayo
imejitokeza kwa miezi kadhaa ambapo nchi za Kenya, Uganda na Rwanda
zimekuwa zikikutana, kujadili na kuafikiana katika masuala yanayohusu
EAC kama usafiri, visa, forodha na mengine yanayoaminika kuwa ni sehemu
ya mambo yaliyokwishajadiliwa au kukubaliwa na EAC.
Hatua za nchi hizi zimezua hisia kwamba Tanzania
na Budundi zimekuwa zikitengwa. Kabla ya Kikwete kutoa msimamo, suala
hili liliibuliwa bungeni na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, akitoa msimamo wa awali wa serikali, kuhusu mshikamano wa
nchi hizo tatu.
Si kusudi la makala haya kuchambua msimamo wa
Tanzania kuhusu mgogoro huo, bali kuhoji kwa nini Tanzania, kama nchi,
imeachia usukani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na si tu kujiweka katika
kiti cha nyuma, bali kwenye daraja la tatu katika ‘basi linaloelekea
kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki?’
Kwa wale ambao wameshuhudia awamu zote nne za
uongozi wa nchi hii watakuwa na faida ya kulinganisha jinsi serikali za
awamu zote zilivyoshughulikia masuala mbalimbali, hasa kuhusu jirani
zetu.
Awamu ya Kwanza iliwajengea Watanzania moyo wa
kujiamini. Walipambana vilivyo, kitaaluma na kiuweledi na wenzao wa
Kenya na Uganda. Tanzania haikuwa na hofu juu ya nchi hizi. Kwa hakika
ilikuwa ni mfano wa kuigwa kwa wapenda maendeleo wote ndani ya Kenya na
Uganda, baadhi ambao walihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Msingi huo wa kujiamini ulijengwa na viongozi wa awamu hiyo.
Tangu awamu hii ya nne ishike hatamu, tumeshuhudia
viongozi wakiwatia hofu raia wa Tanzania kuhusu masuala ya ardhi na
ajira. Eti tukifungua mipaka jirani zetu watafurika na kupora ardhi
yetu. Eti ufunguaji wa mipaka yetu utawaleta jirani zetu kuzinyakua
nafasi za ajira na vijana wetu kubaki bila kazi.
Haya yanasemwa na viongozi wetu wa ngazi za juu.
Kwanza, suala la ardhi limetiliwa chumvi sana na wanasiasa. Hakuna nchi
yeyote ya Afrika Mashariki iliyo na sheria kali kuhusu umiliki wa ardhi
kama Sheria ya Ardhi ya Tanzania. Kwa mujibu wa sheria hiyo mtu asiye
raia hawezi si tu kumiliki ardhi, bali hata nyumba nchini Tanzania.
Hata wale tunaowaita wawekezaji wanamilikishwa
ardhi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na miliki hiyo, hubaki
mikononi mwa kituo. Kwa misingi hiyo, hata tukifungua mipaka, haitakuwa
rahisi kwa mgeni kuja na kumiliki ardhi bila kufuata taratibu
zilizowekwa kisheria.
Katika nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda,
Mtanzania anaweza kwenda huko akanunua nyumba bila tatizo. Kwa mantiki
hii, hofu zinazoenezwa na wanasiasa wetu hazina msingi.
Katika suala la ajira ni lazima tukiri kuwa
viwango vya elimu nchini mwetu vimeshuka sana na hakuna juhudi zozote
zinazoonekana kuibadilisha hali hii.
Nimesikia baadhi ya wawekezaji, hasa kwenye
hoteli, wakilalamika kuwa vijana wa Kitanzania hawajui Kiingereza na pia
ni rahisi kwao kuajiri vijana kutoka Kenya. Labda hali hii ya kuajiriwa
kwa Wakenya katika sekta zetu inaweza kutugutua kutoka kwenye hali hii
ya kuridhika na mfumo wa elimu yetu
No comments:
Post a Comment