Rais Jakaya Kikwete akimfaliji Mke wa marehemu Dk Sengondo Mvungi, Anna Shayo, nyumbani kwa marehemu, eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameeleza
kushtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi kilichotokea juzi kwenye
Hospitali ya Millpark, Johannesburg, Afrika Kusini.
Mwili wa Dk Mvungi unatarajiwa kuletwa kesho na
mazishi yake yamepangwa kufanyika Jumatatu ijayo, Kisangara, Wilaya ya
Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ambaye pia ni msemaji
wa familia, James Mbatia alisema mipango ya kuleta mwili wa Dk Mvungi
ilikuwa inakwenda vizuri ikiratibiwa na Balozi wa Tanzania nchini humo,
Radhia Msuya na mwanaye Dk Mvungi, Deogratius Mwarabu.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa
Rais Kikwete alimtumia salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Jaji Joseph Warioba na kueleza kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa
za kifo cha Dk Mvungi.
“Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa hakuna shaka kuwa katika
maisha yake, Dk Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya
Tanzania kwa namna mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la
Tanzania lilikuwa bado linahitaji busara, hekima na mchango wake katika
mchakato mzima wa kusaka Katiba Mpya.
Aongoza waombolezaji
Rais Kikwete jana aliongoza maelfu ya waombolezaji
kutoa pole kwa familia ya Dk Mvungi nyumbani kwake Kibamba-Msakuzi, Dar
es Salaam.
Rais Kikwete ambaye alifuatana na mkewe, Salma
alitia saini kitabu cha maombolezo na kumpa pole mjane wa Dk Mvungi,
Anna Shayo na ndugu na jamaa wengine kabla ya kuzungumza faragha kwa
muda na Jaji Warioba ambaye alikuwapo msibani hapo pamoja na wajumbe
karibu wote wa tume yake.
Viongozi wengine waliokuwapo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Naibu wake, Angela Kariuki.
Pia kulikuwa na mamia ya waombolezaji wakiwamo wakazi wa maeneo ya jirani, wanasiasa, wasomi na viongozi wa Serikali.
No comments:
Post a Comment