Ni kufuatia hotuba aliyoitoa mwishoni mwa wiki kuhusu
hali tete iliyoanza kujitokeza katika Jumuiya hiyo inayojumuisha nchi
Tano.
Dar es Salaam. Ikiwa ni siku nne
baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge mjini Dodoma akilalamikia
kutengwa na nchi washirika Afrika Mashariki,Kenya imekuwa ya kwanza
kutamka hadharani kushirikiana na Tanzania.
Rais Kikwete katika hotuba yake,alielezea
kushangazwa na washirika wenza wa Afrika Mashariki,Kenya,Uganda na
Rwanda kufanya mikutano ‘kimyakimya’ bila kuwashirikisha.
Inadaiwa baada ya mkutano wa Aprili 28,mwaka huu
mjini Arusha,wakuu hao wa nchi za Kenya,Uganda na Rwanda walikutana
kimyakimya Juni 25 na 26,Entebbe nchini Uganda kabla ya kukutana tena
Oktoba 28, Mjini Kigali,Rwanda katika mkutano waliouita “coalition of
the willing”(Ushirikiano wa hiyari) wenye nia ya ujenzi wa Afrika
Mashariki mpya.
Kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje wa Kenya,
Amina Mohamed, Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu akisema kuwa nchi yake
iko tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba walijiingiza katika
mazungumzo yake na Uganda na Rwanda kuhusu ujenzi wa reli na bomba la
mafuta bila kufahamu kwamba ilikuwa inavunja misingi ya jumuiya hiyo.
Salamu hizo zilizowasilishwa na waziri huyo mbele
ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,alisema kuwa hawaoni
sababu hasa ya kuitenga Tanzania hasa kwa suala la Jumuiya ya Afrika
Mashariki(EAC).
Waziri Amina aliyewasili nchini juzi kuzungumzia
ushirikiano huo alisema, Tanzania na Kenya ndiyo waasisi wa EAC hivyo
hawawezi kuacha ife.
Cuf watoa neno
Chama cha Wananchi (Cuf),kimesema Tanzania itazame
na kuzirekebisha kasoro zinazosababisha nchi washirika wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kuamua kuitenga badala ya kulalamika na kutafuta
huruma.
Mwenyekiti wa Cuf, Profesa ,Lipumba alisema
kumekuwa na kasoro mbalimbali zinazosababisha Tanzania kulalamikiwa na
kufikiriwa kukimbiwa.
Alisema taarifa kuhusu uamuzi wa nchi za Rwanda na
Uganda kutotumia Bandari ya Dar es Salaam lisitazamwe kisiasa badala
yake iangalia udhaifu na upungufu uliopo katika bandari hiyo.
“Rwanda na Uganda si pekee wanaolalamikia Bandari
ya Dar es Salaam bali wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi
zikiwamo Kongo, Zambia na Malawi nao wamekuwa na malalamiko ya muda
mrefu.”
No comments:
Post a Comment