Dar es Salaam. Wakazi wa Tabata na viunga 
vyake, sasa wanaishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na kuibuka kwa kundi 
la vijana, wanaojiita Waasi wakitumia silaha za jadi, kujeruhi watu na 
kupora mali nyakati za usiku.
                
              
Mmoja wa wananchi wa Tabata Matumbi alisema wiki 
mbili zilizopita, vijana hao walimuua mwanamume mmoja kwenye Daraja la 
Reli la Matumbi. Kwa mujibu wa mtoa habari huyo ambaye hata hivyo 
hakutaka jina lake litajwe, mtu huyo alichinjwa na kichwa chake 
kutenganishwa na kiwiliwili.
                
              
“Watu walipeleka kiwiliwili kituo cha polisi, 
maana kichwa hakikupatikana na haikufahamika kama alitambuliwa au vipi. 
Yaani sasa hivi ikifika saa tatu watu inabidi tubaki ndani,” alisema.
                
              
Habari zilisema pamoja na mauaji hayo, pia kumekuwa na matukio ya watu kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao.
                
              
Inasemekana vijana wanaofanya uhalifu huo ni wa umri wa kati ya miaka 14 na 17.
                
              
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Pima 
alisema alivamiwa na kundi la vijana wasiyopungua kumi akiwa nje ya 
nyumba yake. Alisema vijana hao walimkata panga kichwani, baada ya 
kutotii amri yao ya kutaka awakabidhi simu na kila alichokuwa nacho 
mfukoni.
                
              
“Kwanza walipita watoto watatu, wakafuatiwa na 
wengine watatu, mara akatokea mmoja na kunifuata barazani, akanitaka 
nimpe simu, nikahisi anatania maana ni katoto,” alisema Pima.
                
              
Alisema ghafla walitokea wengine wawili na kumwamuru atekeleze amri mara moja.
                
              
Alisema mmoja alijaribu kumpokonya simu, lakini 
akamwahi. Mtu huyo alisema hata hivyo kiongozi wao alimjeruhi kwa panga 
kichwani.
                
              
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msimbazi, 
Beatrice Mukama alisema juzi baadhi ya wananchi wa kushirikiana na 
polisi waliendesha msako uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 16 .
                
              
Alisema watuhumiwa hao wamekabidhiwa polisi-Bunguruni.
 
 
No comments:
Post a Comment