Tuesday 13 August 2013

RAIS KIKWETE AKUTANA NA "WAVUTA BANGI WASTAAFU" IKULU...... AMEITAKA JAMII ISHIRIKI VITA DHIDI YA MADAWA YA KULEVYA



 RAIS Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa ya akili pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini kushirikiana na Kituo cha Ushauri Nasaha cha Pili Misana Foundation, ambacho kinawasaidia waathirika wa madawa ya kulevya ili kiweze kuwahudumia watu wengi zaidi hapa nchini.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema kuwa Rais Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kukutana na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana kilichoko Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa jambo hili, ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote tushiriki katika kulipiga vita” alisema.

Rais Kikwete alimpongeza Pili Misana na Zacharia Hans Pope ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho ambacho tayari vijana wapatao 203 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kuweza kuachana na madawa ya kulevya na kurudia katika shughuli zao za kimaendeleo.

Rais Kikwete amesema tatizo la dawa za kulevya ni la muda mrefu lakini hapo awali lilikuwa halisikiki sana kwa sababu jitihada za kuzuia dawa hizo zilikuwa hazitangazwi wala kufuatiliwa sana.

“Sasa hivi juhudi mbalimbali za kupambana na dawa za kulevya zinatangazwa na hivyo kusikika sana na pia taarifa nyingi zinazohusiana na dawa za kulevya zinawekwa wazi kwa jamii”

Amesema taarifa nyingi zinawekwa wazi na kutangazwa ili kushirikisha jamii katika kupambana na tatizo hili na kwamba serikali inafanya jitihada kubwa kuwasaidia vijana mbalimbali na bado itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi mbalimbali za kupambana na dawa hizo zikiendelea.

Naye mfadhili wa kituo hicho Zacharia Hans Pope ameitaka jamii kushiriki na kuwa karibu zaidi na vijana ili kuweza kusaidia katika mapambano ya madawa ya kulevya na athari zake nchini.


No comments:

Post a Comment