Tuesday 13 August 2013

BILIONEA MWINGINE AUAWA KWA KUPIGWA RISASI JIJINI DAR

Bilionea


MAUAJI ya wafanyabiashara wakubwa ‘mabilionea’ yameshika kasi nchini ambapo baada ya tajiri mkubwa Arusha, Erasto Msuya kuuawa kwa risasi hivi karibuni, Agosti 3, 2013 bilionea Elia Daniel Endeni (49) naye aliuawa kwa kupigwa risasi nje kwa mwanamke anayedaiwa kuwa ni mke wake mdogo aitwaye Juliana Labson (28).
Tukio hilo lilijiri siku hiyo saa 2 usiku maeneo ya Temeke Mikoroshini jijini Dar es Salaam ambako ni nyumbani kwa Juliana.
Elia alikuwa na kampuni iitwayo Elia Herdons Ltd ya kupakua na kupakia mizigo ya makontena bandarini, maduka na majumba ambapo polisi walikuta shilingi 151,000,000 taslimu ofisini kwake akiwa amezihifadhi.
Ilidaiwa kuwa muda huo, Elia alikuwa amefika nyumbani kwa mwanamke huyo lakini kabla hajashuka katika gari lake, Pick-up lenye namba za usajili T 319 AFJ alichomolewa kwenye gari na kupigwa risasi na watu wawili wasiojulikana.
Taarifa zilieleza kwamba waliotekeleza unyama huo walikuwa wakimfuata marehemu huyo kwa nyuma wakiwa kwenye pikipiki.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walisema marehemu alikuwa na kawaida ya kufika nyumbani kwa Juliana nyakati za usiku na kabla ya kushuka kwenye  gari, alikuwa akimpigia simu mwanamke huyo ili afungue mlango.
“Ilikuwa wakati anapiga simu ndipo alivamiwa na watu hao ambao walivunja kioo cha gari kwa kutumia kitako cha bastola kisha kutoa ‘loki’ ya mlango na kumchomoa.
“Walimdhibiti bila kutoa sauti, wakati huo sisi tulikuwa tumekaa nje tukishuhudia lakini tuliamini kwamba huenda walikuwa wamegongana barabarani kwani hata marehemu hakusikika akiomba msaada,” alisema mwanamke mmoja jirani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mwanamke huyo aliendelea kusema kwamba hakukusikika mlio wa risasi, bali marehemu alianza kulia ghafla akiomba msaada.
Aliongeza kuwa watu walipokaribia eneo la tukio, wauaji hao walipiga risasi mfululizo hewani, kitendo kilichowafanya watawanyike kuokoa maisha yao na majambazi hayo yakatoweka.
Inadaiwa majirani walipofika, walimkuta tajiri huyo akiwa amelala katika dimbwi la damu huku ameishiwa nguvu kiasi kwamba alishindwa kuongea chochote.
Habari zinasema mke huyo mdogo aliyezaa naye watoto wawili, alipotoka ndani alizimia baada ya kuona Elia akiwa katika dimbwi la damu.
Muda mfupi baadaye, polisi walifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi kumpeleka Hospitali ya Temeke ambapo alifariki dunia akiwa njiani.
Taarifa zinadai kwamba Julai 28, mwaka huu marehemu Elia alikoswa na risasi akiwa njiani kwenye gari akitokea msibani Same, Kilimanjaro.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Engelbert Kiondo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba walifika katika eneo hilo wakiwa na wasiwasi kwamba huenda watu hao walimnyang’anya bastola.

“Ilitubidi twende ofisini kwake Kurasini na kupekua, tukaikuta bastola. Hili suala linaonekana ni kisasi kwa sababu wamemuua bila kuchukua kitu chochote, tunaendelea na upelelezi,” alisema Kamanda Kiondo.
Mazishi ya Elia yalifanyika Jumatano iliyopita, Same ambapo Juliana alikuwa miongoni mwa waombolezaji. Mke mkubwa wa marehemu aishiye Kimara King’ong’o jijini Dar ndiye aliyekuwa ameongoza msiba huo.

No comments:

Post a Comment