Monday, 27 January 2014

‘Waasi’ sasa tishio kwa wananchi Tabata

Dar es Salaam. Wakazi wa Tabata na viunga vyake, sasa wanaishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na kuibuka kwa kundi la vijana, wanaojiita Waasi wakitumia silaha za jadi, kujeruhi watu na kupora mali nyakati za usiku.
Mmoja wa wananchi wa Tabata Matumbi alisema wiki mbili zilizopita, vijana hao walimuua mwanamume mmoja kwenye Daraja la Reli la Matumbi. Kwa mujibu wa mtoa habari huyo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe, mtu huyo alichinjwa na kichwa chake kutenganishwa na kiwiliwili.
“Watu walipeleka kiwiliwili kituo cha polisi, maana kichwa hakikupatikana na haikufahamika kama alitambuliwa au vipi. Yaani sasa hivi ikifika saa tatu watu inabidi tubaki ndani,” alisema.
Habari zilisema pamoja na mauaji hayo, pia kumekuwa na matukio ya watu kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao.
Inasemekana vijana wanaofanya uhalifu huo ni wa umri wa kati ya miaka 14 na 17.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Pima alisema alivamiwa na kundi la vijana wasiyopungua kumi akiwa nje ya nyumba yake. Alisema vijana hao walimkata panga kichwani, baada ya kutotii amri yao ya kutaka awakabidhi simu na kila alichokuwa nacho mfukoni.
“Kwanza walipita watoto watatu, wakafuatiwa na wengine watatu, mara akatokea mmoja na kunifuata barazani, akanitaka nimpe simu, nikahisi anatania maana ni katoto,” alisema Pima.
Alisema ghafla walitokea wengine wawili na kumwamuru atekeleze amri mara moja.
Alisema mmoja alijaribu kumpokonya simu, lakini akamwahi. Mtu huyo alisema hata hivyo kiongozi wao alimjeruhi kwa panga kichwani.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msimbazi, Beatrice Mukama alisema juzi baadhi ya wananchi wa kushirikiana na polisi waliendesha msako uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 16 .
Alisema watuhumiwa hao wamekabidhiwa polisi-Bunguruni.