Monday 27 January 2014

Wafungwa miaka 56 jela kwa kuharibu mali

Sumbawanga. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Rukwa, imewahukumu watu wanane wa Kijiji cha Sikaungu wilayani Sumbawanga, kutumikia kifungo cha miaka 56 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuteketeza mali za mwekezaji zenye thamani ya zaidi ya Sh 227 milioni.
Akisoma hukumu hiyo jana Hakimu Mkazi Adamu Mwanjokolo, alisema washtakiwa walitenda kosa hilo Oktoba 12 mwaka jana.
Alisema uhalifu huo waliufanya katika kambi ya mwekezaji ambaye ni Efatha Ministry iliyoko Kijiji cha Ulinji ndani ya shamba la Dafco Malonje linalomilikiwa na mwekezaji huyo.
Hakimu Mwanjokolo alisema washtakiwa wamehukumiwa kwenda jela miaka saba kila mmoja.
Aliwataja watu hao kuwa ni Alexander Kisanko, Julius Kazembe, Paul Kazikulima na wenzao watano ambao waliruka dhamana wakati kesi ikiwa mahakamani.
Mwanjokolo alisema ushahidi wa mashahidi sita umethibitisha kwamba watuhumiwa kwa pamoja walivamia kambi hiyo na kuchoma moto matrekta mawili na magunia 188 ya mahindi.

No comments:

Post a Comment