Wednesday, 17 April 2013

Suala la wake za bilionea Sambeke laghubikwa utata



 Ndege aina ya Cessna  5H-QTT  ikiwa imeanguka eneo la Kisongo,  karibu na Uwanja wa Ndege Arusha  juzi jioni, baada ya kugonga mti wakati ikijiandaa kutua  na kusababisha kifo cha mmiliki wake na aliyekuwa rubani, Bob Sambeke(katika picha ndogo juu). Picha na Filbert Rweyemamu 

Wanawake wote watatu wanadaiwa tayari wamewasili Arusha na kwamba, taratibu za mazishi zilikuwa zinendelea vizuri  
Arusha. Wakati mwili wa  bilionea maarufu Ernest Babu ‘Sambeke’ ukitarajiwa kuagwa rasmi  leo Arusha, utata umegubika kuhusu idadi ya wake wa marehemu baada ya taarifa kudai kuwa alizaa na wanawake watatu tofauti  enzi ya uhai wake.
Hata hivyo, Msemaji wa familia,  Dk Richard Masika alisema juzi kuwa marehemu ameacha mke mmoja, Marcelina Sambeke na watoto watatu.
Dk Masika alitaja majina ya watoto wa marehemu kuwa, ni  Siah, Getrude na Jamal ambaye amefuata taaluma ya baba yake  ya urubani, hivi sasa yuko Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akichukua fani hiyo.
Taarifa hizo zinadai enzi za uhai wake, marehemu hakupenda kuishi na  wanawake hao  bali alipenda kuishi na watoto wake muda wote hadi anakutwa na mauti.
Mmoja wa ndugu wa karibu na marehemu, alidai kuwa Sembeke hakupenda kuishi na wanawake hao kwa sababu kipaumbele chake kilikuwa kimeegemea kwa watoto wake.
Mmoja wa wanawake wanaodaiwa kuzaa na Sembeke, Leila Ally mkazi wa Kilimanjaro, alikiri kuzaa naye mtoto aitwaye Jamal ambaye hivi sasa anachukua fani ya urubani.
“Mimi ni mzazi mwenzake, nimezaa naye mtoto mmoja anaitwa Jamal,” alidai Leila kwa huzuni.
Akisimulia historia yake, Leila alisema waliwahi kuishi na marehemu wilayani Moshi na kuna wakati aliwahi kwenda nchini Kenya kuchukua masomo ya urubani.
Suala la idadi ya wanawake waliozaa na marehemu limeonekana kuzua utata katika msiba huo, taarifa za ndani zinadai kuwa baadhi ya wanafamilia wameanza kuhisi huenda likazua tafrani katika mirathi.
Pia, Jamal alipotafutwa alikiri kuwa miongoni mwa watoto wa marehemu, huku akisema ameamua kufuata fani ya baba yake.
Hata hivyo, Dk Masika alipoulizwa iwapo watoto hao ni wa mama mmoja, hakutoa majibu ya uhakika.

No comments:

Post a Comment