Monday, 10 February 2014

Kocha wa Mgambo aelezea jinsi alivyoifunga Simba

Dar es Salaam. Kocha wa Mgambo Shooting, Bakari Shime ameanika siri ya kikosi chake kuitungua Simba bao 1-0 katika pambano baina ya timu hizo lililopigwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Akizungumza na Mwananchi, Shime alisema timu yake iliishinda Simba kwa vile wachezaji wake walijituma muda wote na kucheza kama timu bila kutegemea uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
“Kabla ya mchezo niliwaambia wachezaji wangu Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine hivyo tunachotakiwa kufanya ni kucheza kitimu yaani kwa ushirikiano.
“Niliwaambia kila mchezaji wa Simba wamuone ni hatari si kuelekeza nguvu kuwakaba Tambwe na Messi (Ramadhani Singano) pekee na kweli tulifanikiwa,”alisema Shime.
Aliongeza:”Unajua tatizo la timu nyingi zikikutaka na Simba akili zao zinafikiria kuwadhibiti kina Tambwe na Messi matokeo yake zinafungwa kirahisi, lakini ukiangalia jana (juzi) sisi tulikimbia sana uwanjani kuliko Simba.”
Kocha huyo wa zamani wa timu ya vijana ya Coastal Union alisema makali ya timu yake yataendelea kuziathiri timu nyingine itakazokutana nazo.
“Tumedhamiria kubaki kwenye ligi, tumejiandaa kwa ajili ya timu zote za Ligi Kuu,”alisema Shime.